Ayubu

Chapter 23

1 Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,

2 Hata leo malalamiko yangu yana uchungu; Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu.

3 Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona, Nifike hata hapo anapokaa!

4 Ningeiweka kesi yangu mbele yake, Na kukijaza kinywa changu hoja.

5 Ningeyajua maneno atakayonijibu, Na kuelewa hayo atakayoniambia.

6 Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake? La, lakini angenisikiliza.

7 Hapo waelekevu wangepata kuhojiana naye; Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele.

8 Tazama, naenda mbele, wala hayuko; Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona;

9 Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona; Hujificha upande wa kulia, hata nisimwone.

10 Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.

11 Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka.

12 Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,

13 Lakini yeye ni mmoja, ni nani awezaye kumgeuza? Tena nafsi yake ilitakalo, ndilo afanyalo.

14 Kwani yeye hulitimiliza hilo nililoamriwa; Tena mambo mengi kama hayo ya pamoja naye.

15 Kwa hiyo naona taabu mbele ya uso wake; Nitakapofikiri, namwogopa.

16 Kwa maana Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia, Naye Mwenyezi amenitaabisha;

17 Maana sikufadhaishwa kwa sababu ya giza, Wala kwa sababu giza kuu limenifunika uso.